Saturday, September 10, 2011

MAVAZI GANI HAYA

By Ali Mwero

“Waenda chuo kikuu, maisha huko ni ya kufurahisha sana lakini wakati mwingine huwa shubiri, kwa hivyo hadhari”, hivyo ndivyo mulamu alinitahadharisha na kunishauri. Mnamo tarehe kumi mwezi wa saba nilifika mji wa Eldoret. Baridi kali ilinifanya ni tetemeke ja kifaranga. Wakati huo huo mtima wangu ulikuwa wenye bashasha belele kwani nilitamani kuyaona na kuyashuhudia mazingira ya chuo kikuu cha Moi

Baada ya kusajiliwa, nilijipa moyo wa kufanya matembezi ya hapa na pale ili kujifahamisha na mazingira ya chuo hiki kikuu.Ama kwa kweli ninavumilia na kuyameza mate machungu kwa mavazi niyashuhudiayo. Wengi watasema mimi ni limbukeni lakini katika hali halisi wenye mavazi hayo ndio waliobobea katika ulimbukeni na kujishusha hadhi.

Siku ya kwanza nilipokutana na ‘Getrude’ alikuwa amevalia mavazi nadhifu na yakupendeza si haba. Heshima na kongole nilimpa, nilitamani kumuongelesha lakini niliogopa kuaibika hadharani. Cha kushangaza, baada ya majuma mawili kutoka siku tuliyosajiliwa ‘Getrude’ nilimuona amevalia suruali ndefu iliyombana mapajani na juu alikuwa na bilauzi ambayo haikumsetiri tumbo lake. Aliponisongelea kunisalimu, alijaribu kujinyoosha mwiliwe, salale! Niliduwaa huku mtima ukinienda mbio . Niliyoyaona si ya kuhadithiwa bali kila insi anaelewa bayana.

Si hayo tu, siku nyingine nilipomuona alikuwa amevalia kaptula ambayo iliacha nyonga zote peupe. Bilauzi aliyovalia ilifanya maziwa yake kuonekana. Nilishangaa ghaya na tangu siku hiyo sikuwa na hamu hata ya kumuangalia binti huyo. Chuki dhidi yake ilinijaa na kunifanya kumtema ‘Getrude’ kwenye moyo wangu. Iwapi tofauti kati yetu na wanyama????

Huu ni mfano tu, lakini kunayo mengi ambayo yanitia kiwewe ndiposa uozo katika jamii hautokoma abadan katan.Ningewasihi dada zetu wajipe hadhi kwa kuvaa mavazi mwafaka na ya heshima. Mungu si Athmani! Siku utakayokutana na Israeli ndiyo siku utakayokumbuka maisha yako na haswa mavazi yako.

Najua inawachoma sana, lakini sina budi kuufungua ukurasa mpya wa hisia zangu. Japo ni chuo chenye tofauti lakini tofauti yenu ya mavazi inatia wahaka nyoyoni mwa wengi. Kwa wale wanaokereka mtaniwia radhi kwa sababu huu ni mwanzo na mwanzo wa ngoma ni lele


No comments:

Post a Comment

your comment, your voice...

Search site.