Tuesday, September 13, 2011

Ole wao wote

by Quintas Wasonga
Wakati mwingine mimi husoma Bilbilia haswa vifungu vinavyoeleza kuwa Yesu mwana wa mungu alikuwepo hapa duniani na akafa kwa ajili ya dhambi za walimwengu na huwa ninashangaa sana licha yangu kuwa na imani dhabiti ya kikristu.Hoja si kuja wala kufa kwake bali ni wakati ambapo alikufa.Kuna mhubiri mmoja ambaye tulikubaliana katika fikira aliposema kuwa iwapo mungu hataadhibu kizazi hiki haswa karne ya ishirini na moja,basi anafaa kuomba msamaha kwa wananchi wa Sodoma na Gomora.

Baadhi ya dhambi ambazo yasemekana zilikuwa zimemuudhi mungu siku hizo,hivi leo tumepiga hatua zaidi.Je mungu atakuwa mwenye hasira kiasi gani kuona mabasha na wasenge wakifungishwa ndoa makanisani na hata wengine wao wakitawazwa kuwa maaskofu? Ole wao siku hiyo ya kiama itakapofika baada ya wateule (mimi na wengine wachache) kunyakuliwa.Nawaambieni mapema ,ole wao!

Maandiko matakatifu yatueleza vyema kuwa pesa ndio msingi wa maovu yote ulimwenguni.Kanuni hii imegeuzwa na siku hizi hata ibada ya dakika kumi sharti ikamilike kwa matoleo “kwa mungu.”Laiti waumini hawa wangejua ni vipi “mungu” huyo hutumia pesa hizo.Siku hizi hata kuna wengine ambao sadaka hutumwa kwa M-pesa au moja kwa moja katika benki;jinsi mambo yaendavyo kinyume.Ukiuliza hili, utaambiwa mkono wako wa kushoto usijue kile mkono wa kulia umetoa.Ole wao!

Yesu mwana wa mungu alitoa wosia wazi kwa wale ambao wangependa kuingia ufalme wa mbinguni:lisha wenye njaa,visha wasio na nguo,watembelee wagonjwa . . . Hivi leo wakenya wafa njaa na baridi katika kambi za wakimbizi huku wahubiri na viongozi wa kidini wakikusanya pesa za kununua mafuta ya magari yao ya bei ghali .Ole wao!

Mungu alimlalamikia Haggai akisema ,”Nyumba yangu imekuwa magofu huku nyinyi mkijijengea makasri.”Leo hii utakuta makanisa yenye paa bila ukuta au ukuta bila paa na hata mengine ni ya makaratasi ilhali waumini wamevalia suti na kuegesha nje magari makubwa na utawasikia wakisema bila haya “Bwana asifiwe.”Kumbuka pia imeandikwa kwamba maombi ya mwenye dhambi ni kelele mbele za bwana.Ole wao !

Iwapo kumbukumbu la torati lifafwatwa,basi wengi wa kina dada zetu wataangamia mara moja.Mwanamke amekatazwa kuvalia nguo za wanaume wala kujaribu kujilinganisha na mumewe.Mtume Paulo akiwaandikia wakorintho pia anasisitiza haya.Bibilia imewekwa kando na inayotawala ni mkataba wa Beijing.Licha haya,yatembelee makanisa jumapili hii na ujionee jinsi itakuwa rahisi kuteua wachache wa kuingia mbinguni.Ole wao !

Nyimbo nzuri za kumsifu na kumuabudu mungu enzi za Daudi zimegeuzwa kuwa za kisasa ndiposa ziwavutie wasikilizaji.Siku hizi hata mahubiri sharti yapambwe kwa lugha ya kuvutia hadhira hata kama yanamuudhi mungu.Imewabidi wahubiri kuwaambia waumini kile ambacho wangependa kusikia badala ya kueleza ujumbe wa mungu ambao wanapaswa kusikia.Usishangae ndugu mpendwa Yesu mwana wa mungu akija na kurejea mikono mitupu kwa kuwa ulimwengu mzima umepotoka pasiwe hata mmoja mkamilifu mithili ya Sodoma na Gomora.Ole wetu !

No comments:

Post a Comment

your comment, your voice...

Search site.