Wednesday, October 5, 2011

SI KUPENDA KWANGU

by ASIDAGA (MALENGA MKARIRI)

Jina langu ni Klombod Omene. Wengi hunitambua kama Kamoshi. Siku za hivi majuzi, maisha yangu yamefunikwa kwa wingu kubwa la huzuni. Upweke pia umepiga kambi kwangu na katu haubanduki. Sina wa kunena naye ndiposa nikaamua kuandika kifungu hiki. Hasa ningependa kuwaeleza mambo ambayo yamenijiri muhula huu.

Juzi nilijaribu kuzungumza na kidosho mmoja ili nimweleze yaliyokuwa moyoni. Mara bila kutarajia alinikatiza na kusema kuwa mdomo wangu ulikuwa unavunda kama kaburi la maiti. Alisisitiza kuwa, hangedhubutu nililokusudi kwa sababu hakuona lolote la maisha ya usoni nami. Kana kwamba hakutosheka, alinieleza kuwa tabasamu langu lingerudisha nyoka pangoni. Si kupenda kwangu, mimi hujaribu kupiga mswaki.

Tangu juma lililopita sijahudhuria mhadhara wowote kwa sababu ya kisa kilichotokea katika mhadhara wa mwisho niliohudhuria. Dada mmoja mrembo aliyekuwa amekaa kando alizirai ghafla bin vuu. Alipelekwa zahanati na kufanyiwa huduma ya kwanza akapata nafuu. Daktari alisema kuwa mrembo huyo alikuwa amekosa hewa safi ndiposa akazirai. Maneno haya yalinikumbusha mwingine aliyehisi kichefuchefu baada ya kukaa kando yangu kisha akaenda nje kutapika. Si kupenda kwangu. Mimi hujaribu sana kukumbuka kukoga.

Mikosi iliendelea kuniandama mtawalia. Nilihudhuria kikundi chetu cha somo la saikolojia siku ya Jumamosi. Kufikia wakati huo watu wengi walikuwa wamejua mchango wangu mzuri katika utunzi wa mazingira.

Wanakikundi waliponiona nikija, walianza kujitayarisha kwa kufunika mapua yao kwa vitambaa. Haya hayakunishika mishipa kwa sababu nilikuwa nimezoea. Nilizidi kuenda na nilipofika walikuwa wakarimu na kunipa kiti, kalamu na karatasi ili niandike yote watakayoyajadili. Agizo la mwisho lilikuwa nisifungue mdomo; ninyamaze tu na kuandika. Baada ya muda mfupi wa mjadala, niligundua kila mtu alikuwa anatazama jinsi nilivyokuwa nikiandika.

Nilikuwa nikitetemeka mikono na jasho lingi lilikuwa linanitoka kwenye vidole vyangu vyeusi. Karatasi lote lilikuwa limeloa jasho.

Kule chumbani wenzangu wamenitoroka. Waliafadhalisha kuishi kama wakimbizi kuliko kuishi na mimi. Waliteta kuwa hawakuweza kupata hata lepe la usingizi kutokana na kukohoa kwangu usiku mzima. Walishuku naugua T.B: jambo lililowapa sababu ya kutorudi hata kidogo. Huo si ukweli, sikuwa na T.B. Naugua saratani ya mapafu!

Hata hivyo, nini jambo ninalojivunia? Sijawahi patwa na maradhi madogomadogo kama malaria kwa sababu mbu nao pia hawangeweza kustahimili harufu mbaya na moshi wa sigara.

Ninaenda kuzimu. Huko hakutakuwa na haja ya kununua kibiriti cha kuwasha sigara.

Si kupenda kwangu, ni shetani!!

No comments:

Post a Comment

your comment, your voice...

Search site.